Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kujenga tabia ya kuwa wanapima hali zao za lishe ili kuweza kuepukana na magonjwa yasiyoambukizwa kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, utapiamlo n.k
Kauli hiyo imetolewa na Bi Pili Kassim ambae ni Afisa Lishe wa Manispaa hii wakati wa zoezi la upimaji wa lishe lililoratibiwa na Kitengo cha Lishe cha Manispaa ya Ilemela siku ya tarehe 21 Agosti lilioenda sambamba na upimaji wa presha kwa lengo la kujua hali za lishe la watumishi sambamba na kutoa elimu ya lishe bora kwa watumishi hao kulingana na hali zao za lishe.
“Sisi kama watumishi wa idara ya afya tumeona kuna haja ya kupima hali ya lishe kwa watumishi kwani wengi wao hawana muda wa kufuatilia hali za lishe kutokana na majukumu mengi walionayo, Hivyo tumeamua kuwaletea huduma hii karibu”, Alisema
Aidha Bi Pili amewasisitiza watumishi kujenga tabia ya kupima hali zao za lishe mara kwa mara angalau mara moja kwa mwezi, kuzingatia ulaji unaofaa pamoja na kufanya mazoezi kwa kufanya hivi kutaepusha magonjwa mbalimbali
Kwa mujibu wa Afisa Lishe Joyce Albert amesema kuwa upo umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya lishe kwa watumishi na wananchi kwa ujumla ili kuweza kuimarisha hali zao la lishe aidha ameongeza kusema kuwa kwa mujibu wa vipimi hivyo vya lishe watumishi wengi wamekutwa na uzito uliokithiri na kuwahimiza kujitokeza kupima hali zao za lishe pindi fursa kama hizi zinapojitokeza
Nao watumishi wa Manispaa ya Ilemela katika nyakati tofauti wamepongeza kwa zoezi hili la upimaji wa hali ya lishe kwani wengi wao walikuwa hawana elimu ya kutosha ya lishe bora, sambamba na hilo wameshauri kuwa zoezi hili liwe endelevu kwa kuongeza na vipimo mbalimbali.
Bi Chami David Sollo ni mtumishi wa Divisheni ya Utawala upande wa utunzaji wa kumbukumbu yeye amesemea kuwa, kupitia zoezi hilo ameweza kupata elimu juu ya namna bora ya kuzingatia ulaji wa vyakula na kufanya mazoezi kitendo ambacho kitawakinga dhidi ya magonjwa sambamba na kuomba zoezi hilo kuwa endelevu kwani lina manufaa kwa wengi
Bi Joyce Kanuda ambae ni Mwanafunzi wa Field amepongeza zoezi hilo na kusema kuwa hapo awali alikuwa akikabiliwa na ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya namna bora ya kuzuia unene usiofaa kwa afya yake sanjari na kujua juu ya namna bora ya kuzingatia makundi ya chakula hivyo kushukuru kwa elimu iliyotolewa huku akiwata watumishi wengine kutumia elimu iliyotolewa kwa ufasaha majumbani mwao
Nae Bi Rhoda Nyamsenda kutoka ofisi ya utunzaji wa kumbukumbu, amesema kuwa imekuwa kawaida yake kufika hospitali kwa ajili ya kupima afya yake na kusema kuwa amefurahia kwa zoezi hili kusogezwa eneo la kazi kwani imewarahisishia kuendelea na kazi sambamba na kujua hali yake ya lishe kutokana na kwamba haitamlazimu kutoka katika eneo la kazi kwa ajili ya kwenda kujua hali yake ya lishe.
Florence Vedasto wa divisheni ya Maendeleo ya Jamii yeye amesema ameamua kufika kupima kwa sababu alitaka kujua uzito wake na kulinganisha na urefu, aidha amesema kuwa amejifunza namna ya ulaji wa watu wengi sio mzuri huku akishauri vipimo vingine viongezeke ili kuwezesha watumishi kujua hali zao za Afya, na pia amewahimiza watumishi wenzake kujitokeza kupima fursa kama hizi zinapojitokeza
Juma Kingh’ola ni mtumishi wa Divisheni ya Miundombinu alisema kuwa yeye amesema amejifunza mengi ambayo alikuwa hayafahamu ikiwemo matumizi bora ya chakula kuweza kujikinga na uzito uliokithiri na magonjwa yasioambukizwa
“Ukizingatia matumizi bora ya lishe unaweza kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kama vile presha lakini si hivyo tu utajikinga na uzito uliokithiri,” Amesema Ndugu Juma
Kwa mujibu wa Bi Pili amesema kuwa zoezi hili litakuwa endelevu na halitaishia kwa watumishi wa makao makuu bali litafika hadi ngazi za Mitaa ambapo kwa upande wa watumishi wa Makao Makuu zoezi hili litafanyika kila robo ya mwaka ambapo kwa upande wa watumishi waliopo ngazi ya kata zoezi litafanyika mara mbili kwa mwaka.litakuwa ni endelevu ambapo litakuwa linafanyika kila robo ya mwaka
Takriban watumishi 60 walijitokeza kupima hali zao za lishe, huku watumishi 20 wamekutwa na uzito uliokithiri wapo pia waliokutwa na hali nzuri ya lishe na wapo pia wenye uzito uliokithiri ambapo wote hao walipatiwa elimu ya namna nzuri ya ulaji wa vyakula.