Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo ameongoza Kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe katika Mkoa wa Mara na kuwataka viongozi, watendaji na wataalamu kufanya maboresho katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Mtanda amewataka Maafisa Lishe wa Halmashauri kutekeleza kikamilifu majukumu yao ili kuwasaidia Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na watendaji wengine katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe.
“Ninyi mkitekeleza majukumu yenu vizuri, mtawakumbusha viongozi wenu na kuwapa tahadhari mapema wakati wa utekelezaji ili kuzitoa Halmashauri katika utekelezaji hafifu wa mkataba huu muhimu kwa ustawi wa jamii”amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda pia amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia utekelezaji wa mkataba wa lishe hadi ngazi za vijiji, mitaa na kata na tarafa ili kuweza kuwafikia wananchi katika maeneo hayo.
Aidha, Mhe. Mtanda ameziagiza Halmashauri kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinakuwa na ubao wa kupimia urefu ili kuviwezesha vituo hivyo kupima hali za afya za wananchi wanaopata huduma za matibabu katika vituo hivyo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu ameeleza kuwa Mkataba wa Lishe katika baadhi ya Halmashauri hautekelezwi vizuri kwa sababu fedha za masuala ya lishe zinatengwa katika vyanzo ambavyo havina uhakika.
“Halmashauri nyingi zinatenga fedha za kutekeleza mkataba wa lishe kutoka katika mapato ya ndani au fedha za wafadhili vyanzo ambavyo havina uhakika sana na hivyo kusababisha utekelezaji hafifu wa Mkataba wa Lishe” amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu ameeleza kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali, fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe zisipotolewa katika mwaka wa fedha husika zinapaswa kuwa deni katika mwaka wa fedha unaofuata ili kutekeleza shughuli zilizokuwa zimepangwa.
Kwa upande wake, Afisa Lishe kutoka Sehemu ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Bwana Benson Sanga ameeleza kuwa Halmashauri ziangalie uwezekano wa kutenga fedha za kuwawezesha Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ili kuwawezesha kutoa elimu kuhusu masuala ya lishe kwa wananchi.
“Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii wakiwezeshwa wanaweza kupita nyumba kwa nyumba na kutoa elimu kwa mtu mmoja mmoja ambayo mtu ataisikiliza zaidi kuliko njia za mikutano ya hadhara inayotumika sasa ni njia ngumu kuweza kuwabadilisha wananchi” amesema Bwana Sanga.
Bwana Sanga ametoa mfano wa Halmashauri ya Chunya ambayo Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wametengenezewa vitambulisho, wamewapatiwa tisheti na kuwanunulia baskeli kwa awamu ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Huu ni mfano mzuri wa kuigwa ambapo pamoja na kusaidia kuwawezesha wahudumu hawa, pia umewafanya watambulike kiurahisi katika jamii na kuwajengea kujiamini wanapotekeleza majukumu yao yakiwemo masuala ya lishe” amesema Bwana Sanga.
Kikao cha tathmini ya Mkataba wa Lishe kimehudhuliwa na Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Sehemu na Vitengo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Halmashauri, Maafisa Lishe, Waweka Hazina, Maafisa Utumishi na Maafisa Mipango wa Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara.