Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Masasi wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Agosti 16, 2023, Afisa lishe wa Halmashauri ya Mji Masasi, Bi. Happiness Mlamka amesema lengo mahususi la elimu hiyo ni kuwakumbusha wazazi, walezi na jamii juu ya umuhimu wa afya na lishe kwa mtoto.
“kipekee kabisa tumekuja kwenye adhimisho la siku ya afya na lishe ya Kijiji. Siku hii imelenga kuwakumbusha wazazi, walezi na jamii kwa jumla juu ya umuhimu wa afya na lishe kwa mtoto lakini pia kwa jamii nzima, mambo yaliyofanyika leo tumetoa elimu juu ya unyonyeshaji wa Watoto kwa miezi sita hadi miaka miwili, lakini pia tumetoa elimu ya makundi Matano ya chakula, namna sahihi ya kuandaa mlo kamili kwa vile vyakula vinavyopatikana katika jamii kwa vitendo” Bi. Mlamka
Aidha amesisitiza umuhimu wa wanaume kuhudhuria matukio ya elimu ya afya na lishe kwa kuwa ni jukumu la wazazi wote kuhakikisha lishe bora inapatikana.
“leo tumepata baadhi ya wanaume, tunaendelea kutoa wito wanaume wote tuendele kujitokeza kwa kuwa zoezi hili ni la wote” Afisa lishe.
Kwa upande wake, Afisa mtendaji wa Kijiji cha Mayula Bw. Alex Mwambwalwa amesema idadi ya wazazi waliofika katika elimu hiyo imefanikiwa kutoka na uhamasishaji uliofanyika na mwamko wa wazazi juu ya umuhimu wa lishe kwa Watoto.
“wananchi tulionao hapa wanatoka katika Kijiji cha Mayula na Kijiji cha Mbonde na Idadi ya Watoto waliohudhuria ni takribani Watoto 200” Bw. Alex
Mmoja kati ya baba aliyefika akiwa na mtoto wake kupata elimu hiyo, Bw. Samweli Abdalah mkazi wa Kijiji cha Mayula, amewahimiza wazazi wa kiume kujitokeza kwa wingi katika matukio ya elimu za afya na lishe zinazotelewa na watalaamu ili kuwezesha malezi bora ya Watoto.
“ Mimi natokea kata ya Mwenge mtapika, kijiji cha Mayula, nimekuja kujifunza juu ya kumlea mtoto kuhusu uji wa lishe, nawakaribisha wazazi wenzangu jukumu la kumlea mtoto sio la wanawake pekee yake, tujitahidi sana kuhudhuria sana kwenye hii mikusanyiko, tunajifunza mambo mengi sana” Bw. Samweli.
Katika kuhakikisha lishe bora inapatikana utekelezaji wa mpango wa upatikanaji wa chakula shuleni unatekelezeka kwa vitendo katika kata hiyo ikiwemo kupata mafanikio katika shule ya msingi Mbonde kwa kulima, kuvuna na kukusanya mazao kama mbaazi, mahindi na alizeti.