Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Dkt Christopher Timbuka amesema Jumla ya Kilo Mia Tisa za Mbegu Daraja la Uthibitisho (certified seed) zimegawiwa katika vikundi 17 kutoka katika Kata zote 17 za Wilaya ya Siha na jumla ya kilo 4500 zimevunwa na kusambazwa kwa wakulima ili kuzalisha Nafaka.
Mhe. Dkt Timbuka amesema hayo leo Agosti 16, 2023 katika Ufunguzi wa Mafunzo kwa Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule, Maafisa Elimu Kata, Maafisa Kilimo wa Kata na Afisa Elimu Msingi na Sekondari yaliyotolewa na Serikali kwa kushirikiana na Taasisi isiyokuwa ya Serikali ya Global Alliance for Improved Nutrition (Gain) katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Siha.
Amesema Jumla ya Kilo 1200 za Maharage Lishe zimevunwa katika Wilaya ya Siha baada ya kuwasambazia wakulima mbegu zilizothibitishwa na wakulima kujipatia chakula na kipato.
Dkt. Timbuka amewataka Maafisa Kilimo na Lishe ngazi ya Wilaya,Kata na Vijiji kuendelea kusisitiza matumizi ya mazao yenye virutubisho ili kutimiza lengo la Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Taanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan la kujenga Taifa lenye afya bora.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Dkt. Haji Mnasi amesema ataendelea kusimamia utekelezaji wa mikataba ya lishe na maelekezo ya Serikali ili kuondokana na changamoto za kiafya zinazotokana na ukosefu wa lishe bora.
Baada ya uzinduzi wa mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Siha Dkt Christopher Timbuka amekabidhiwa mbegu za Maharage zenye virutubisho na Taasisi isiyokuwa ya Serikali ya Global Alliance for Improved Nutrition (Gain) na kuzikabidhi kwa Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha.