Katika kuhakikisha tatizo la udumavu kwa watoto waliochini ya miaka mitano linaondoka divisheni ya lishe Halmashauri ya Mji Bariadi imeendelea na zoezi la utolewaji wa elimu ya lishe bora kwa wananchi ili kusaidia katika ukuaji wa mtoto kiakili na kimwili kufuatia uzingatiaji namna bora ya kuandaa lishe bora ya mtoto kwa kujumuisha makundi matano muhimu ya vyakula yanayohitajika.
Afisa Lishe Halmashauri ya Mji Baraidi Bi.Fatuma Kombo amewataka wazazi kuhakikisha wanazingatia na kufuatilia afya ya mtoto kila mara ili kuwa na uhakika wa namna ya ukuaji wake huku akiwataka wazazi kuhakikisha wanazingatia makundi yote matano wakati wa kuandaa chakula cha mtoto kwani makundi yote hayo yana umuhimu mkubwa katika ukuaji wa mtoto.
Awali akitoa elimu ya maandalizi ya kuchanganya makundi yote matano kwenye chakula cha mtoto Afisa Muuguzi wa Halmashauri ya Mji Bariadi Bi.Yustina Feya amesema ili mtoto aweze kukua vizuri ni vema kuzingatia makundi ya chakula anayopatiwa mtoto kwani kutozingatia lishe ya mtoto inasababisha udumavu na kuwa na mtoto asiyekuwa na afya bora na kupelekea ukuaji wake kuwa wa kusuasua .
Mtaa wa Bupandagila na gisadi kata ya nyakabindi imeadhimisha siku ya afya ya lishe kwa kupatiwa elimu sahihi ya namna bora ya kuandaa lishe ya mtoto na umuhimu wa kuzingatia lishe hiyo katika ukuaji wa mtoto ambapo katika maadhimisho hayo shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwemo utolewaji wa elimu sahihi ya lishe pamoja na utolewaji na huduma mbalimbali kwa watoto ikiwemo huduma ya upimaji uzito,kupima mzunguko wa kati wa sehemu ya juu ya mkono kwa kutumia MUAC Tape,utolewaji wa matone ya vitamin A na chanjo .