Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere amewataka viongozi na wananchi wote kuendelea kuutumia ujuzi juu ya lishe bora walioupata kupitia mafunzo yaliyotolewa na Shirika la Lishe Endelevu wakati wa utekelezaji wa mradi wake wa Lishe Endelevu. Mradi huo umetekelezwa Mkoani Rukwa kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia Mwaka 2018 na unatarajiwa kuisha Septemba 2023.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa shughuli zilizokuwa zikifanyika na Lishe Endelevu, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amesema lishe inapaswa kuwa agenda endelevu pamoja na kuwa ufadhili wa Shirika la Lishe Endelevu unakoma Mwaka 2023.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amelishukuru na kulipongeza Shirika la Lishe Endelevu kwa kuwajengea uwezo Watendaji wa Kata, Maafisa Kilimo, wanawake vinara, wahudumu wa afya, wahudumu wa afya ngazi ya jamii, wakulima na wafungaji juu ya masuala ya lishe bora.
Kuongezeka kwa uelewa wa wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuhusu kulima na kula mchanganyiko wa vyakula unaozingatia lishe bora, kunyonyesha watoto kwa kipindi cha miezi sita bila kuwapa kitu kingine chochote na kunawa mikono kwa maji yanayotiririka ni miongoni mwa mafanikio ambayo Mkoa unajivunia.
Mkoa wa Rukwa ulishika nafasi ya kwanza Kitaifa katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa Mwaka 2022.