Na Stella Pantaleo; Bukoba DC
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mheshimiwa Erasto Sima amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Bukoba kwa jitihada wanazofanya katika kutekeleza mikataba ya afua za lishe kwa wananchi wa Halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Sima ametoa pongezi hizo wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri hiyo pamoja na wadau wa lishe waliopo katika kata mbalimbali za Halmashauri hiyo katika kikao cha tathimini ya usimamizi wa mkataba wa afua za lishe ngazi ya jamii kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Pongezi hizi zinatokana na jitihada zilizofanywa na uongozi wa Halmashauri hii kupitia kwa watendaji wa kata katika kuhakikisha utekelezaji wa mkataba wa kusimamia wa Afua za Lishe ngazi ya jamii unafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani kwa mujibu wa takwimu za Halmashauri, mafanikio ya utekelezaji wa afua hizo yameongezeka kutoka asilimia 83.71 ya mwezi Oktoba – Disemba mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 93.8 mwezi Januari- Machi mwaka 2023.