Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga imeibuka kinara wa utekelezaji wa Afua za Lishe kwa kipindi cha Mwaka 2022/2023 na kukabidhiwa cheti cha pongezi na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere. Halmashauri hiyo imeongoza katika kwa kutenga fedha na kusimamia utekelezaji mipango na bajeti ya lishe. Fedha zilizotumika katika masuala ya lishe katika Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa Mwaka 2022/23 ni asilimia 128.
Akikabidhi cheti cha pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Bi. Lightness Msemo, Mheshimiwa Makongoro ameitaja Halmashauri hiyo kama mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe na kueleza kuwa Mkoa wa Rukwa unaweza kuwa wa kwanza katika masuala mengine pia ikiwa yatapewa kipaumbele kama ilivyofanyika kwa suala la lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amezitaka Halmashauri zote kutenga fedha na kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika kwa kuzingatia mipango iliyowekwa. Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zingine zote za Mkoa wa Rukwa kujifunza na kuiga mbinu zinazotumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Akihitimisha hafla hiyo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amezielekeza Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa kusimamia ipasavyo mipango na bajeti zilizowekwa. Ametaka kusimamiwa kwa mpango wa shule kuwa na mashamba na bustani za mbogamboga ili kusaidia upatikanaji wa chakula bora kwa wanafunzi huku akaielekeza kuongezwa kwa viini lishe katika chakula kinachosambazwa na wazabuni wa shule na huku akisisitiza kutungwa kwa Sheria Ndogo za lishe kwa kila Halmashauri.