Katibu Tawala wa Wilaya ya Maswa Ndg. Athuman Kalage amewataka wakuu wa Divisheni zote zinazohusika na masuala ya lishe wahakikishe kuwa katika vikao vyao ajenda ya lishe iwe ya kudumu na waandae mpango kazi ambao utawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi katika kutekeleza shughuli zote za lishe Bora kwa kuwa wao ndio wanabeba ajenda hiyo.
Katibu Tawala alisema hayo katika kikao cha Kamati ya lishe Wilaya kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa chenye lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2023 ambapo Divisheni zinazohusika na utekelezaji wa afua hizo ziliwasilisha taarifa zao.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya elimu ya awali na Elimu msingi Dkt. Lucy Kulong’wa alisema kuwa Divisheni hiyo ilipewa kiasi cha shilingi Milioni 3 na Laki Tisa kwa ajili ya kutekeleza afua za lishe katika shule 135 za Msingi katika Wilaya ya Maswa lengo ni kuhakikisha shule zote zinatoa chakula kwa wanafunzi shuleni na kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwepo utoaji wa Elimu katika shule zote 135, kupanda miti ya matunda pamoja na mbogamboga.
“Tumefanikiwa kutoa Elimu kwa walimu pamoja na maafisa Elimu Kata juu ya uhamasishaji na utoaji wa Elimu ya utoaji wa chakula mashuleni, tumefanikiwa kwa 95% ya shule 135 zinatoa chakula pamoja na uji mashuleni.” Amesema Dkt Lucy.
Pia ameongeza kuwa upatikanaji wa huduma ya chakula mashuleni utasaidia ufaulu wa wanafunzi kuongezeka.
Afisa lishe wa Wilaya ya Maswa Ndg. Abel Gyunda amewataka maafisa Elimu wa Wilaya kuwasisitiza walimu wakuu na wakuu wa shule kupeleka mahindi yao katika mashine yenye virutubishi vya lishe ambapo lengo likiwa wanafunzi hao wapate chakula chenye virutubishi vya aina nne ambavyo vitawasaidia kupata mlo kamili utakaowasaidia kufikili vizuri na kufanya vizuri katika masomo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Ndg. Robert Urassa alisema katika utekelezaji wa afua za lishe Divisheni hiyo imehamasisha wakulima katika vikundi vya vijana na wanawake juu ya umuhimu wa ulaji wa mahindi lishe, viazi lishe, matumizi ya mbogamboga, sambamba na kuendesha mafunzo ya usindikaji wa mahindi kwa kuweka virutubishi kwenye unga wa mahindi (fortification) .
Aidha Ndg Urassa amesisitiza kuwa Divisheni imetoa Elimu juu ya unywaji wa maziwa kwa kuadhimisha siku ya maziwa duniani katika shule 10 za msingi ambapo wanafunzi wamepewa Elimu ya umuhimu wa maziwa mwilini na kuwashauri watumie glasi moja ya maziwa kila siku pamoja na kula vyakula vyenye lishe bora.
Mratibu wa lishe Divisheni ya Elimu Sekondari Ndg. Mathayo Maingu alisema mpango wa lishe katika shule za Sekondari ulilenga kuanzisha Bustani za mbogamboga na matunda lengo likiwa ni kuongeza thamani ya chakula kwa wanafunzi ambapo shule zote zilipata Elimu hiyo ambayo iliongozwa na Afisa Lishe wa Waliya kwa kuhamasisha uanzishaji wa Bustani hizo na kuanzisha klabu za lishe ambazo zitasaidia kuendelea kuhamasisha ufanyikaji wa shughuli za utunzaji wa Bustani hizo ambapo shule 16 zimefanikiwa kuanzisha Bustani za mbogamboga na zingine kushindwa kutokana na changamoto ya ukame.
Nae Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Bi. Basila Bruno alisema Divisheni yao imetekeleza afua za lishe kwa kutoa Elimu kuhamasisha wananchi kula vyakula vyenye virutubishi vyote vyenye kuhusisha makundi yote matano ya lishe ambapo Elimu ya lishe bora imetolewa kwa wananchi 1878 wanaume 1020 na wanawake 858 katika Kata zote 36 kwa akina mama wajawazito, watoto, akina mama wanaonyonyesha, wazazi na walezi pamoja na wanafunzi katika shule tofautitofauti.