Kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imefanya kikao Jumuishi cha Lishe na kujenga uwezo kwa wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma. Kikao hicho pia kimetumika kuwasilisha utekelezaji wa shughuli za Lishe kwa kipindi cha robo ya nne ya April – Juni, 2023. Kikao hicho kimefanyika tarehe 13 Julai, 2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Kikao kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mh. Salum Kalli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe ya Wilaya. Katika ufunguzi wake Mh. Mkuu wa Wilaya amesisitisha elimu na ufuatiliaji wa afua za lishe ili kuwa na jamii yenye afya bora. Kikao hicho pia kimehudhuliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bi. Rose Robert Manumba. Katika kutekeleza afua za Lishe, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bw. James Swai amebainisha kutolewa kwa bajeti ya Lishe inayotokana na mapato ya ndani katika afua za Lishe.
Miongoni mwa mambo ambayo Mratibu wa Lishe ameweza kuyafanya katika kipindi cha robo ya tatu Januari – machi, 2023 ni pamoja na: Utoaji wa dawa za kuongeza wekundu wa damu (FeFo) kwa wanawake wajawazito waliohudhuria clinic, Kupima uwepo wa madini joto kwenye chumvi inyouzwa sokoni na inayotoka kwenye jamii kupitia wanafunzi shuleni, kufanya Siku ya Afya na Lishe (SALiKi) katika vijiji 45, Kushiriki kufanya kampeni ya kitaifa ya mwezi wa afya na lishe ya mtoto n.k.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na wataalamu wa idara ya afya kutoka ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma pamoja na Mratibu wa Lishe kutoka OR-TAMISEMI Bw. Mwita Waibe amabaye pia alitoa maelekezo ili kuweza kufanikisha Afua za Lishe. Bw. Mwita Waibe alisisitiza umuhimu wa kuwa na data zenye ubora ili ziweze kusaidia katika maamuzi sahihi.